Maana ya Hadithi
Hadithi
m kazi ya sanaa inayotumia lugha. Kwa hiyo, hadithi, yaweza kuwa masimulizi ya
kubuni ama ya kweli yaliyo katika nathari. Sanaa hiyo ya hadithi ni kazi ya mtu
yenye mwigo wa uyakinifu uliofungamana na wakati, mazingira na mfumo wa jamii.
Kwa sababu hii, utanzu huu unaweza kupatikana katika fasihi zote zilizopo
katika jamii: fasihi simulizi na fasihi andishi.
Katika
ujenzi wa hadithi, binadamu hutumia akili kuiga maisha kisanaa. Mwigo katika
hadithi hizo buzingatia kanuni na taratibu za uzuri, upendezaji, uozo na ubaya,
na kwa hiyo huathiri hadhira katika kuvuta ama kuchukiza nulango ya fahamu ya
mwanadamu. Kama kazi ya sanaa, fasihi husawiri maisha ya jamii inayohusika. Kwa
sababu ya kusawiri huko, hadithi inalazimika kueleza tukio, mahali na wakati
ambapo tukio hilo hutendeka, watenzi wa tukio (wahusika) na hatimaye mbinu za
kulieleza tukio hilo, n.k. Masimulizi yanayokuwa katika hadithi yanaweza
kumhusu mtu mmoja ama yanaweza kuwahusu watu wengi. Masimulizi hayo yanahusu
juu ya mambo yaliyotokea, au mambo yanayoweza kutokea katika jamii.
Uwezo
wa kiakili anaokuwa nao binadamu, ni ule wa kuiga maisha, ambao kimsingi mtu
anazaliwa nao. Tofauti yake na wanyama ambao nao kwa kiasi fulani wana uwezo wa
kuiga maisha ni kuwa bmadamu uwezo anao mkubwa zaidi wa kuiga kuliko viumbe
wengine. Kutokana na mambo ya awali ya kielimu, hasa lugha; ambayo hatimaye
huitumia katika shughuli mbalimbali za maisha yake, ikiwa ni pamoja na
uandishi; mwanadamu huwa juu ya viumbe wengine hai.
Hadithi
hutofautiana kutokana na uwezo wa msanii na lengo ama mazingira ambayo hadithi
hiyo Husimulia au kuandikwa. Katika msingi huo, uwezo wa fanani ama mwandishi
ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa fani na maudhui ya hadithi. Hadithi hizo
huzingatia kanuni ama taratibu maalumu za kisanaa. Hali hiyo huifanya hadithi
iwe tofauti na kazi nyingine za kisanaa ama zisizo za kisanaa zinazotumia
lugha.
Hadithi
kama kazi ya kisanaa hutumia lugha yenye semi, tamathali za usemi, nahau na
kadhalika, ili kuwasilisha matendo na mawazo ya wahusika. Tamathali na semi
husaidia kuitofautisha hadithi kama kazi ya sanaa na kazi nyingine zitumiazo
lugha ambazo si za kisanaa na zimeandikwa kwa ujazo. Tamathali hufanya hadithi
isiwe mazungumzo ya kawaida, bali huifanya kazi ya sanaa inayosawiri maisha na
inayozingatia kanuni na taratibu maalum kama tulivyodokeza awali.
Kwa
upande mwingine, hadithi huweza kupambanuliwa na kazi nyingine za sanaa
zitumiazo lugha kama vile ushairi na tamthiliya. Utanzu wa ushairi kwa mfano,
una umbo tofauti na umbo la hadithi. Utanzu wa tamthiliya pia unatofautiana na
hadithi kwa misingi kuwa tamthiliya katika uandishi wake huzingatia sana
kipengele cha utendaji jukwaani, lakini hadithi lengo lake mara nyingi huwa ni
kusomwa tu. Tena, wakati shairi haliwezi kuingiza kitu katika muundo wa
usimulizi wake, hadithi na tamthiliya zinaweza kuingiza mashairi na nyimbo
katika kuimarisha fani na maudhui yake. Vipengele hivyo ndivyo hufanya hadithi
iwe tofauti na tanzu nyingine k'ama vile ushairi na tamthiliya kwa misingi kuwa
inao uwezo wa kutumia tanzu nyingine zote za kifasihi.
Ufafanuzi
huu ni wa jumla, lakini unatuelewesha waziwazi hadithi ina umbo gani. Sasa
hatua itakayofuata ni kufafanua matawi mbalimbali ya hadithi ili tuweze kujua
nafasi ya hadithi fupi.
Hadithi Ndefu na Fupi
Katika
fasihi simulizi ziko hadithi ndefu zinazosimuliwa na kufahamika sana. Lakini
pia kuna hadithi ndefu katika fasihi andishi zenye kuwa na athari nyingi za
dhamira zilizokuwa zikijitokeza katika fasihi simulizi.1 Hadithi
nyingi ndefu za simulizi mara nyingi zilikuwa katika umbo la tenzi kama vile
tenzi za Nanga.2 Hadithi hizo ndefu katika baadhi yajamii,
zilikuwa zikisimuliwa toka asubuhi hadi jioni, na zilikuwa zikihifadhiwa
kichwani tu. Makabila kama ya Wahehe yanasemekana yalikuwa na aina hizi za
hadithi zilizoweza kusimuliwa kwa muda mrefu.3 Kwa sasa
usimulizi wa aina hii hauwezekani tena kutokana na mambo mengi yaliyokumbwa na
mfumo wa kijamii na wa kihistoria.
Kwa
upande wa hadithi ndefu katika fasihi andishi, hizi zinajipambanua zaidi.
Utanzu huu ambao huwa katika maandishi tu ulianza kustawi wakati wa mageuzi ya
viwanda na utamaduni huko Ulaya. Utanzu huu ulizuka baadaye sana ukilinganisha
na tanzu nyingine za kifasihi, kama vile ushairi na nyimbo. F.E.M.K. Senkoro
anasema utanzu huu ulizuka katika wakati maalumu wa historia ya jamii. Wakati
huo, "jamii ilikwisha kuwa kubwa yenye makao maalumu, na lugha ya jamii
hiyo ilikwishapevuka kiasi cha kuweza kueleza dhana, imani na amali mbalimbali za
jamii kwa wasanii wa kinathari: (prose fiction)".4 Ukoloni
na uvumbuzi ulileta hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa hadhira pana zaidi ya
ile ambayo ilikuwa ikisimuliwa kwa ngano na hadithi kwa ufupi. Hata hivyo, bado
ni muhimu kuieleza maana ya riwayajapokuwa m kwa ufupi tu, ili tuweze kutumia
maelezo hayo wakati wa kuipambanua hadithi fupi.
E.
Mphahlele, akitoa maana ya riwaya kwa ujumla, vilevile anakadiria jumla ya
maneno yanayotumiwa katika hadithi kuwa ni mojawapo ya kipimo chake cha riwaya.
Anasema, "... kati ya maneno 35000 na 50000 tunapata riwaya fupi. Biwaya
ndefu ama riwaya kamili ni ile ya maneno 75000..."5 Lakmi
anakiri pia kuwa si lazima kila mara iwe hivyo. Kwa upande mwingine, ufafanuzi
huu kimsingi hauzingatii ukweli uliopo wa riwaya za Kiswahili
ambazo nyingi zma maneno chini ya idadi anayoisema Mphahlele.
Kwa
mujibu wa Penina Muhando na Ndyanao Balisidya, hadithi ndefu ni "fani
(utanzu) yenye umbo maalumu. Umbo hili, pamoja na kujengwa katika vipengele
vingi ndani yake, lina usanifu unaoifanya hadithi ... isiwe maongezi tu au
maandishi ya kawaida."6 Kauli hii ikichambuliwa inaonyesha
kuna mambo mengi yanayoiunda riwaya.
Senkoro
anasema kuwa riwaya "ni kisa ambacho ni kirefu vya kutosha, chenye zaidi
ya tukio moja ndani yake. Ni kisa mchangamano ambacho huweza kuchambuliwa na
kupimwa kwa uzito na undani wake kwa mambo mbalimbali kimaudhui na kifani ...
kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti vingi kama apendavyo
mwandishi wake."7 Ufafanuzi huu kimsingi hautofautiani na
ule uliotolewa na Penina Muhando na Ndyanao Balisidya.
Sifa
ya uchangamano inaonyesha kuwa ni muhimu katika kuielezea hadithi. Aidha,
tatizo linalojitokeza katika dondoo hili la Senkoro linahusu utata unaotokana
na matumizi ya maneno "kisa kirefu" na "hadithi ndefu"
pamoja. Tatizo kubwa ni kutambua tofauti ya msingi baina ya kisa kirefu na
hadithi ndefu. Je, pengine tunazungumzia dhana moja, ambayo imekuwa ikitumia
maneno hayo katika nyakati mbalimbali? Na kwa upande mwingine, ikiwa
tutakubaliana na ufafanuzi wa Muhando na Balisidya, au Senkoro, tuna hakika
kuwa hadithi fupi za Kiswahili zitakuwa na sifa zilizo tofauti, au zilizo
kinyume na hizo za riwaya. Japokuwa kauli hii ina ukweli fulani, hapa kuna haja
ya kuipambanua zaidi hadithi fupi.
Ngano: Hadithi Fupi za Fasihi Simulizi
Kwanza
tutaanza na kuziangalia hadithi fupi katika fasihi simulizi. Katika aina hii ya
fasihi, hadithi fupi ambazo hujulikana rasmi kwa istilahi ya "ngano,"
ni nyingi na zimekuwa zikihifadhiwa kwa kichwa na kutolewa kimasimulizi kutoka
kizazi hadi kizazi. Baada ya kugunduliwa kwa maandishi, hadithi hizo
zilihifadhiwa kimaandishi, hata katika lugha ya Kiswahili tunayo mifano mingi.
Tutazmgatia ngano hizo andishi hasa na kuona uhusiano wake na hadithi fupi za
kisasa. Tunapofanya hivi tunaamini kuwa kuna kuchukuliana tabia na kuathiriana
ama kufanana kwingi kimaudhui na kifani kati ya ngano na hadithi fupi za kisasa
za Kiswahili. Baada ya kusoma sehemu inayohusu ngano na ile inayohusu hadithi
fupi, tutaona tofauti kati ya tanzu hizi mbili za hadithi. Hapa tuanze na
kuielezea maana ya hadithi fupi ya kimapokeo, yaani, ngano, kama
inavyofafanuliwa na wanataaluma na wanafasihi mbalimbali.
Wataalamu
wengi, akiwemo J. Berg Esenwein, wamepata kutoa maana ya ngano kwa ujumla.
Esenwein anasema kuwa:
...ngano ni masimulizi
yaliyorahisishwa (Simple narrative), kwa kawaida masimulizi
hayo ni mafupi yasiyo na muundo kama wa hadithi za kawaida. Masimulizi hayo
tena hutumia wahusika bapa na hutegemea matakwa ya fanani katika kujenga
vitendo mbalimbali kuliko muundo katika kuwajenga wahusika.8
Halafu Esenwein anajaribu kuzigawa ngano katika mafungu kadhaa. Mafungu hayo ni
ya ngano-adilishi, ngano-furahishi, na kundi la mwisho linajumuisha aina mbili
za ngano zilizotajwa awali. Mgawanyo huu umefanywa kwa kuzingatia dhamira
zinazotumiwa na ngano hizo. Kwa mujibu wa Esenwein, mgawanyo huu ni wa jumla
mno na ngano hizi zikiangaliwa kwa undani bila kujali mgawanyo huu uliosemwa
zitaonekana bado zina muundo rahisi.
Aidha,
mwanafasihi na mhakiki Ruth Finnegan9 anazigawanya ngano katika
makundi ya jumla mawili kufuatana na wahusika wanaotumika. Kundi la kwanza ni
la ngano zitumiazo wahusika-watu na la pili ni la wahusika-wanyama. Finnegan
anasema kijumla na kifupi tu kuwa ngano za wahusika-wanyama ni fupi,
zinasisimua na zinakejeli. Ngano zinazotumia wahusika-watu nazo ni nyingi na
huwa kwa kawaida ni ndefu kidogo kuliko zile za wahusika-wanyama. Hata hivyo,
mgawanyo huu pia nao ni wa jumla. Migawanyo midogo midogo ya aina hii si muhimu
kwa sasa. Tutazingatia mgawanyo wa msingi ulio mpana.
Ngano
hazina mshikamano kama ule wa hadithi fupi za kisasa za Kiswahili katika ujenzi
wa vipengele vyake mbalimbali. Ngano huonekana kama kitukio (Episode) wakati
mwingine kilichochukuliwa kutoka tukio moja kubwa ili kukidhi haja fulani ya
kiadili katika jamii.
Jambo
la msingi linalojitokeza hapa ni kuwa ngano ni hadithi za simulizi za mapokeo,
si za kubuniwa wala hazichukui mandhari na mazingira ya kiuhalisia. Kauli hii
ya kubuni inahitaji ufafanuzi zaidi. Tunaposhikilia suala la kubuni hapa
tunasema kuwa katika hadithi za kingano mtunzi ama msanii si lazima ajulikane
kwa hadhira, bali la msingi ni yale maadili ambayo kila mwanajamii anayo haki
ya kuyaeneza katikajamii na kutoka kizazi hadi kizazi. Japokuwa inawezekana
kabisa hadithi hizo za kingano kwanza zilibuniwa, lakini kwa vile hazijabuniwa
upya bali zimesimuliwa upya katika mazingira mapya, kwa sasa tunasema kuwa
ngano hazibuniwi lakini hadithi fupi za kisasa zinabuniwa na kujikita katika
mazingira ya kihalisia. Kwa upande mwingine, japokuwa ngano ni za mapokeo;
fanani anao uwezo wa kuingiza vitu vya kubuni ambavyo kwa asili yake havikuwa
katika masimulizi ya awali. Na haditbi fupi za kisasa nazo zinaweza kutumia
vipengele vingi vya kifasihi-simulizi. Kwa sababu hii, Esenwein anakiri katika
ufafanuzi wake wa hadithi fupi kuwa:
... lazima ifahamike
kuwa kuna magazeti siku hizi (wakati huo wa 1909) yanayochapisha ngano nzuri
sana ambazo zinaweza kuwa na kipengele kimoja, viwili ama vitatu na zaidi
ambavyo vinapatikana katika hadithi fupi. Kadiri vipengele hivyo vinavyozidi
kuweko katika ngano, ngano huelemea zaidi kwenye hadithi fupi na hivyo huwa
vigumu wakati mwingine kuzitenganisha tanzu hizi.10
Suala la muda nalo ni muhimu katika usimulizi wa ngano. Ngano, kwa kiasi
kikubwa hutumia muda ambao ni wa wakati uliopita usio na mpaka (Infinite
past). Ndiyo maana tunapata hadithi zenye mianzo kama "Hapo
zamani za kale..." Kale hii ni ipi? Upi ni mpaka wa ukale na usasa? Au
utasikia, "Zamani zile za mababu..." Mababu wepi? Ni zama zipi hizi
za mababu, na ni wapi huko? Kwa hakika kuna matatizo makubwa kama tunataka
kuuainisha muda wa ngano.
Kwa
sababu ya kutumia muda uliopita usio na mpaka, ni vigumu kujua mandhari ya
hadithi hizo kwa ufasaha kabisa. Katika hali halisi, tunashindwa kuhusisha
historia yajamii na hadithi hizo kikamilifu.
Tukimwacha
Esenwein, ufafanuzi mwingine wa maana ya ngano umetolewa na Penina Muhando na
Ndyanao Balisidya. Kulingana na ufafanuzi wao, ngano ni aina "maalumu ya
hadithi ipatikanayo katika fasihi asilia ya jamii yetu, fasihi ambayo ilitumia
zaidi akili na ubongo wa binadamu kwa kuhifadhiwa kwake."11 Halafu
wanafasihi hao wanaeleza pia muundo wa ngano na maudhui yake. Wanasisitiza
kuwa:
Ngano nyingi aghalabu ni
fupi na kutokana na ufupi huo, hizi si hadithi zinazoinglia mambo kwa undani
sana. Hadithi hizo huingia moja kwa moja katika kulitoa wazo kuu, na kila
kipengele kiijengacho ngano: wahusika, vielelezo na mizungu mingineyo huelemea
katika wazo hilo.
Tabia ya ufupi iliyotajwa hapo awali inapatikana katika hadithi fupi za kisasa
pia.
Tumeona
kuwa baada ya kufika kwa maandishi, baadhi ya hadithi hizo za kingano zimepata
kuandikwa. Ngano andishi zinatofautiana na ngano simulizi hasa katika kutoa
athari ya maana ama mjengo wa sanaa. Kutokana na kuandikwa, mambo kama vitendo,
nyimbo na sauti zake, ming'ong'oso na vidoko n.k., haviwekwi katika ngano kwa
sababu si rahisi kufanya hivyo. Katika usimulizi wake, ngano simulizi zinapewa uzito
wa kisanaa kwa sauti na matendo. Vitu kama nyimbo na mashairi kadha wa kadha
huingizwa pia, vitendawili na methali ama mafumbo mengine, n.k.
Tumekwisha
ona kwamba wanyama, mimea, wadudu, miti n.k. ndio wanaokuwa wahusika katika
ngano. Kadiri siku zilivyoendelea matumizi ya wahusika binadamu yaliingizwa.
Hata hivyo hawa wahusika wa ngano walichanganywa na wahusika wanyama ama
miungu, n.k. Wahusika wa ngano, kama wanavyosisitiza Robert Scholes na Robert
Kellogg, "ni bapa na mara nyingi hawabadiliki kama vile kukua, kuugua
ama kufa katika mkondo mzima wa hadithi. Wakati mwingine wahusika wanakuwa
wawakilishi wa makundi mengine ya watu katika jamii."13 Wahusika
wa namna hii hutumika kama vielelezo na ni wachache mno ukiwalinganisha na wale
wa hadithi fupi. Vilevile, wahusika wa ngano mara nyingi hawapewi majina; bali
hutokea kama, "Mtu na mkewe ..." au ''Zamani za Mfalme..." au
"Paliondokea mtu mmoja..." Mhusika mkuu wa ngano ni muhimu sana. Yeye
ndiye anayekuwa kiungo na ndiye anayebeba ujumbe wa hadithi nzima. Wakati
mwingine, wahusika wa ngano sio lazima wawe wa kuaminika. Hii ni kwa sababu
ngano mara nyingi hazijengwi katika ulimwengu ama mazingira halisi, zinaweza
kujengwa katika ulimwengu wa majini, mizimu, miungu, n.k. Tukilinganisha na
hadithi fupi katika kipengele hiki, tunaona kuwa hawa wa hadithi fupi za kisasa
wanaumbwa kwa mapana kidogo kuliko wale wa ngano, tena ni wa kuaminika. Wasanii
wa hadithi fupi za kisasa wanatumia mbinu za kidrama katika usanii wao. Jambo
hili ni tofauti na mbinu za kingano.
Tumedokeza
hapo awali kwamba ngano ni fupi kuliko hadithi fupi ya Kiswahili ya kisasa. Hii
ni kwa sababu hadithi hizo za ngano hueleza mambo yake kimkato mno
ukilinganisha na hadithi fupi za kisasa. Ngano pia husisitiza masimulizi yale
yenye lengo la kutoa uzito mkubwa kwa maadili ambayo fanani anapenda yafike kwa
hadhira iliyokusudiwa. Kwa mfano, kama fanani analeta dhamira ya choyo, basi
ngano nzima itaelekezwa kimasimulizi kwenye ubaya wa uchoyo. Na hivyo ndivyo
huwa tabia ya ngano karibu zote.
Inasemekana
kwamba ngano zilikuwa za kwanza kuzuka katika jamii baada ya wimbo wa kazi na
ushairi. Ngano nyingi zilihusu mazmgira yaliyomzunguka binadamu kwa ujumla. Kwa
upande wa maudhui, F.E.M.K.Senkoro14 anasisitiza kuwa ngano za
mwanzo zilihusu mazingira na visa-viini. Masimulizi mengi kama vile ya
kichawichawi yalizidi. Ngano hizi, kwa kutumia imani mbalimbali za kidini na
kichawi zilisimuliwa nyakati za jioni (tena pengine wakati wa kufanya kazi
isiyo nzito). Ngano hizo pia zilihusu chanzo cha mtu na chanzo cha dunia.
Kulikuwa pia na ngano kuhusu matambiko, uzazi, jando na unyago na nguvu za
miungu mbalimbali, vifo n.k. Ngano hizi zilishamiri sana. Umuhimu wa ngano
uliwekwa katika maadili ziliyotoa. Kwa sababu hii, kama tulivyokwisha kudokeza
hapo awali, suala la watunzi wake halikutiliwa mkazo sana. Hapakuwa na ulazima
mkubwa sana kwa mtunzi wa ngano kujulikana, lakini maadili yake yalipaswa
kujulikana kwa jamii na kutumiwa vilivyo. Sasa tuangalie utanzu wa hadithi fupi
za Kiswahili.
Hadithi Fupi za Kisasa
Baadhi
ya wananadharia na wanafasihi, hasa wale wenye mapokeo ya hadithi fupi andishi
za huko Ulaya na Marekani wamezipambanua hadithi fupi za kisasa kwa
kuzilinganisha na utanzu wa hadithi ndefu, ama riwaya. Kufanya kwao hivyo
kunatokana na madai na mtazamo wao kwamba tanzu hizi mbili zinahusiana na
kufanana katika baadhi ya mizungu yake ama katika baadhi ya mbinu zake za
uandishi na hata kuwasilisha maudhui yake katika jamii.
Japokuwa
kuna ukweli katika kauli hii, hadithi fupi andishi katika mapokeo ya fasihi
andishi ya Kiswahili zina sifa na misingi muhimu inayozipambanua na kuzifanya
zionekane tofauti na tanzu nyingine kama vile riwaya. Viko vigezo vingine vya
msingi vinavyozipambanua hizi hadithi fupi ambavyo hutumiwa na wanataaluma mbalimbali
katika kuelezea maana ya hadithi fupi kwa ujumla. Tutavijadili vipengele hivyo
hapa chini.
Hadithi
fupi za kisasa zinabeba uzito wake mkubwa sana katka kipengele cha kubuniwa na
kinachosemwa na kuandikwa mara nyingi huelemea kwenye matendo yale ya kihalisia.
Pamoja na kubuniwa huko, bado wakati mwingine kuna athari za kifasihi simulizi.
Patricia Mbughuni anakiri jambo hili kwa kusema kuwa:
...fasihi ya Kiswahili
ya sasa ina athari ya fasihi simulizi kisanaa na kimandhni. Mambo kama dhamira,
mtindo na muundo ama ujenzi wa wahusika pamoja na falsafa zilizokuwa
ziaajitokeza katika fasihi simulizi zinajitokeza pia katika fasihileo ya
Kiswahili japo kama kuna mambo kadhaa yamebadilika.15
Bila shaka mabadiliko hayo yanatokana na mfumo wa historia katika jamii ambao
hubadilika kufuatana na wakati.
Kwa
mujibu wa Rajmund Ohly,16 athari mbalimbali zilizoko katika
fasihileo ya Kiswahili zinatokana na hali ya mazingira. Kwanza, athari hizo
zimetokana na mapokeo ya mifumo mbalimbali katika utamaduni, uchumi na siasa.
Athari hizo zinaambatana na mtindo wa kutoa maadili ya kidini. Kuna kundi la
pili la athari ambalo linatokana na ujio wa wageni katika sehemu hii ya Afrika
Mashariki. Athari hizi zinatokana na mataifa ya Asia, Oman na Shiraz, pamoja na
zile za mataifa ya Magharibi. Athari ya tatu inayojipambanua katika hadithi za
fasihi za kisasa ni ile inayotokana na nafsi-jenzi ya waandishi wenyewe. Hapa
ina maana kwamba kama mwandishi ni mwanamke, maandishi yake yatakuwa na athari
kadhaa za msingi ambazo ni za kike, na kama mwandishi ni mwanaume, athari
kadhaa za msingi zitakuwa zile za kiume. Kwa hiyo tunategemea kuona dhana kama
vile madai ya ukombozi wa mwanamke, athari ya mitazamo ya vijana kuhusu maisha
na pia mitazamo ya wazee ama watu wa makamo. Tunategemea pia kuona athari za
kielimu katika baadhi ya kazi za kifasihi zitakazotolewa na watu wa jamii ya
sasa.
Tulisema
pale awali kuwa hadithi fupi za kisasa zinatakiwa ziwe za kubuni, na kwamba
kipengele hiki ni muhimu. Aidha, yako mambo mengine ya msingi ambayo kusema
kweli yanaifafanua zaidi hadithi fupi ya kisasa. Katika ufafanuzi wake,
Esenwein kwa mfano, anaanza kwanza na kusema kile anachokiona kuwa si hadithi
fupi. Anasema: "...hadithi fupi si kifupisho cha riwaya."17 Baadhi
ya wasomaji na waandishi, hasa wale wachanga, wanashindwa kutofautisha na
kuelewa hadithi fupi ni nini hasa. Kwa sababu hii, wanadhani kuwa hata riwaya
ikifupishwa inaweza kuchukuliwa kama haditbi fupi. Kimsingi, tofauti katika
tanzu hizi mbili zimo kaiika aina na wala sio katika urefu. Urefu ni kigezo
kinachoweza kutumika katika kuziainisha tanzu hizi mbili, lakini kigezo hiki
lazima kishirikishwe na vingine.
Jambo
la pili analoona mtaalamu buyo kuwa si hadithi fupi ni maelezo kuhusu tukio ama
masimulizi kuhusu jambo fulani linalotakiwa kukamilishwa kwa kusimuliwa ama
kuungwa na jingine. Wala hadithi fupi sio sura moja ya riwaya ndefu. Hadithi
fupi ni utanzu mkamilifu unaojitegemea.
Esenwein
anaendelea kukanusha kwamba hadithi fupi siyo madondoo yaliy-otayarishwa kwa
ajili ya kuandika kazi ya sanaa fulani, hususan hwaya au tamthiliya. Wala
hadithi fupi si masimulizi yaliyofupishwa juu ya maisha ya mtu kutoka utotoni
hadi uzeeni. Hadithi fupi ni kazi inayojitegemea na ni yenye sifa zake maalumu
zinazoifanya iwe fupi.
Wakati
mwingine, wako baadhi ya watu wanaoipa ngano uzito na hadhi ya kuwa sawa na
hadithi fupi ya kisasa. Esenwein anasisitiza kuwa kila aina hapa ina misingi
maalumu, japo kuna kufanana kwa kiasi fulani katika vipengele kadhaa. Mtazamo
wake kuhusu hadithi fupi ni upi basi?
Esenwein,
kwa kutumia sifa-hasi zilizotolewa hapo juu katika kuipambanua hadithi fupi,
analeta sifa-chanya ambazo hatimaye zinaupambanua utanzu wa hadithi fupi.
Esenwein18 anatoa sifa zifuatazo za hadithi fupi:
1. Pawepo na tukio moja
lililopewa uzito kuliko jingine lolote. Kwa sababu ya kupewa uzito, mawazo na
mbinu zote kuhusu tukio hilo, zitaelekezwa kwenye tukio hilo, na ujenzi wa kila
kitu huelekezwa kwake.
2.
Awepo mhusika mkuu mmoja anayejitokeza sana kuliko wengine wote katika hadithi
hiyo. Wahusika wengine wasielezwe kwa mapana.
3.
Lazima hadithi hiyo iwe na sifa ya kubuniwa. Sifa hii ikikosekana, tayari kuna
dosari katika kuuainisha utanzu huu wa hadithi fupi. Kubuni sio maana yake
kusema uwongo, hadithi ya kubuni ina ukweli fulani wa maisha.
4.
Hadithi fupi inapaswa iwe na msuko. Pawepo na upangaji mzuri wa maelezo
yanayotiririka kutoka mwanzo wa tukio kutendeka hadi mwisho wa kutendeka kadhia
hiyo.
5.
Maelezo na masimulizi katika hadithi fupi yatumie mawanda yasiyo mapana.
Maelezo hayo yatumie muda mfupi, yatolewe kimkatomkato na kwa kifupi.
6.
Pawepo na umoja na mshikamano wa maelezo katika mtiririko na msuko wa hadithi
nzima. Mshikamano huo lazima ulete mantiki kwa msomaji wa kazi hiyo.
7.
Masimulizi yaonyeshe umoja wa hadithi yote.
Tukiyaangalia maelezo hayo kiundani, yote yana ukweli fulani. Japokuwa kuna
ukweli huo, tuna wasiwasi juu ya maelezo hayo kwa sababu ya shabaha ya uainisho
wake. Esenwein hakufikiria hadithi za Kiswahili katika uainisho wake. Na kusema
hivyo haina maana kuwa sifa hizi zilizotajwa hapo juu juu ya uainisho wa
hadithi fupi, hazifai. Zinaweza kuwa sahihi kabisa. Tunachbhitaji kufanya sasa
ni kuthibitisha kama kweli sifa hizo zipo katika hadithi fupi za Kiswahili kama
zilivyo katika mapokeo ya hadithi fupi andishi za Kiswahili.
Pamoja
na upambanuzi alioufanya Esenwein ambao pia tunaukubali kwa kiasi kikubwa, ziko
nadharia nyingine walizozitumia wataalamu mbalimbali katika kuelezea maana ya
hadithi fupi.
Nadharia
ya kwanza ni ile inayohusu muda. Nadharia hii imepata kutumiwa na baadhi ya
wanataaluma kuelezea maana ya hadithi fupi, hasa katika mapokeo ya fasihi
andishi ya huko Ulaya na Marekani. Nadharia hii inasisitiza kuwa hadithi fupi
iwe ni kitu (maandishi) kinachoweza kusomwa kwa muda mfupi. Hadithi fupi
inatakiwa isomwe katika kikao kimoja. Allan Poe19 ndiye
aliyekuwa miongoni mwa watu walioiendeleza sana nadharia hh. Lakini waanzilishi
wa nadharia hii ni Plato na Aristotle (300 K.M.).20 Wanataaluma
hao walidai kuwa kazi ya sanaa ya kitanzia lazima iwe fupi ili iweze kusomwa
kwa muda mfupi na kukaa akilini mwa watu na kukumbukwa kirahisi. Hii, waliona
wataalamu hao, itawafanya watu waweze kukumbuka maudhui na falsafa zilizomo
kwenye kazi ya aina hii ya kisanaa bila matatizo makubwa.
Wanataaluma
hao pia walisisitiza juu ya mpangilio mzuri wa maneno wakati wa kuandika kazi
ya sanaa ili isomeke kwa urahisi na haraka.
Kwa
miyibu wa Aristotle, kazi zote za tanzia, kwa kuwa zilikuwa ngumu,
zilihitajika, pamoja na mengineyo, kuwa na msuko mzuri (safi) wa visa, fikra
kuu au wazo kuu moja na sahihi ili wasomaji wake wasipate shida. Inawezekana
mtazamo huu umechangia katika kuikuza nadharia hii inayohusu muda katika
kuelezea maana ya hadithi fupi.
Aidha,
katika hali halisi, kigezo hiki cha muda kina matatizo yake. Kwanza kabisa,
baadhi ya wasomaji wa hadithi fupi wanaweza kutumia saa nyingi mno kuliko labda
inavyotakiwa kuisoma hadithi moja fupi kwa sababu hawasomi harakaharaka. Ama
wengine nao wanaweza kutumia muda mchache mno kuliko labda inavyokadiriwa iwe
katika kuisoma hadithi fupi hiyo kwa sababu wanaweza kusoma haraka. Tatizo
kubwa hapa ni kuuainisha muda huu unaosemwa kuwa m mfupi, na kuangalia misingi
inayozingatiwa katika kuisoma kazi inayohusika. Ni kipimo kipi hasa kichukuliwe
kama ni muda mfupi utakaotumika katika kuisoma hiyo hadithi fupi?
Kwa
upande mwingine ziko kazi za kisanaa ambazo zinaweza kusomwa katika kikao
kimoja na kumalizika kwa muda mfupi. Kwa mfano, riwaya iliyofupishwa inaweza
kusomwa yote kwa muda mfupi. Lakini hii haina maana kuwa riwaya hiyo
iliyofupishwa itakuwa ni hadithi fupi. Jambo la muhimu kusisitiza ni kuwa
pamoja na kutumia muda mfupi, lazima pawe na vigezo vingine vitakavyosaidia
kuipambanua hiyo hadithi fupi. Kwa msingi huo, nadharia hii ya muda ni yajumla
mno katika kutoa ufafanuzi wa hadithi fupi ya Kiswahili.
Nadharia
nyingine mayotumika katika kuelezea maana ya hadithi fupi ni ile inayozingatia
idadi ya maneno. William Saroyan21anapendekeza na kuona kuwa hadithi
fupi inapaswa iwe na maneno kati ya elfu mbili mia tano na chini ya elfu kumi.
Ikiwa hadithi itakuwa na maneno chini ya elfu mbili mia tano, basi itakuwa
imechukuliwa kuwa ni hadithi fupi iliyo fupi sana.
Akizungumzia
nadharia hiyohiyo ya wingi wa maneno, Walter Blair na wenzake anasema kuwa
hadithi fupi mara nyingi, "huwa chini ya maneno elfu kumi, lakini mara
chache huwa na maneno zaidi ya elfu thelathini na tano."22 Halafu
anaendelea kwa kusisitiza kuwa "hadithi fupi hukamilika inapokuwa yenye
umoja na mshikamano na uhusiano katika vipengele vyake vyote. Hadithi fupi si
kifupisho cha riwaya ama hadithi ndefu ya aina yoyote ile..."23 Mawazo
hayo yanaelekea kukubaliwa na kuungwa mkono na wataalamu wengine kama vile
Ezekiel Mphahlele na Penina Muhando na Ndyanao Balisidya. Katika kusisitiza
hoja yao, kwa mfano, Muhando na Balisidya wanasema kuwa "visa (hadithi
fupi) ni hadithi zenye fani inayoachana na ile ya ngano kwa undani na uhuru
wake... Aidha, zina urefu ulio pungufu ya ule wa riwaya..."24 Hawatoi
idadi ya maneno.
Tukifuatilia
kwa makini hoja hizo zinazotolewa, tunaona kuwa katika mapokeo ya fasihi
andishi ya Kiswahili, nadharia ya maneno inatofautiana kimtazamo na
ilivyoelezwa hapo awali kama kipimo cha hadithi fupi. Hii inatokana na hoja
kuwa dhana ya "neno" katika lugha za Kibantu, si sawa na dhana ya
neno katika lugha kama vile Kiingereza. Katika lugha za Kibantu, neno linaweza
kuwa na maana ya sentensi kamili.
Zaidi
ya hayo, hadithi fupi za Kiswahili kimsingi hazijawahi kuvuka maneno elfu kumi.
Katika Kiswahili, hadithi zilizokuwa na maneno zaidi ya elfu kumi zimekuwa
zikichukuliwa kuwa m riwaya. Hapajawa na ugumu aghalabu wa kuainisha riwaya.
Mara nyingi imekuwa ni ndefu, fupi au ndogo.
Tukizitazama
nadharia zote hizo, sasa tunaweza kusema kuwa hadithi fupi ya Kiswahili m nini.
Hadithi fupi ya Kiswahili itakuwa na misingi karibu yote tuliyoyadili hapo
awali. Aidha, ili kuikamilisha na kuitambulisha kuwa ni hadithi ya Kiswahili,
mazingira yake ya kifani na kimaudhui yanakuwa yale yaliyojikita katika
utamaduni wa watu watunriao lugha ya Kiswahili.
Vifuatavyo
ni vipengele muhimu ambavyo vinaipambanua hadithi fupi ya Kiswahili:
· Ni masimulizi ya
kadhia moja lililowekwa katika mazingira ya utamaduni wa lugha ya Kiswahili.
· Kadhia hiyo
ielezwe kwa ufupi na isitumie wahusika wengi, mara nyingi mmoja au wawili.
· Hadithi fupi iwe
ni masimulizi ya kubuni. Maana ya kubuni siyo kusema uwongo. Hadithi ya kubnni
ni kiwakilishi cha kisanaa kwa kutumia lugha.
· Hadithi fupi ya
kubuni sio foto ya maisha halisi, bali ni maisha yaliyosan- ifiwa, yaliyorembwa
au kutiwa chumvi kwa shabaha maalumu.
· Hadithi fupi ya
Kiswahili inatakiwa iwe na msuko, tofauti na hadithi za kingano. Maelezo na
mawazo muhimu yawe yamepangwa vizuri
· Hadithi fupi ya
Kiswahili haipaswi kuwa na mawanda mapana kwa namna yoyote ile.
· Hadithi fupi ya
Kiswahili haina mchangamano wa masimulizi. Mandhan huwa si mapana.
Ni muhimu kutambua kuwa baadhi ya sifa hizi zinaweza pia kupatikana katika
tanzu nyingine za kisanaa kama vile riwaya na tamthiliya.

Kielelezo 1: Fasihi na Tanzu Zake
Maelezo
1.
Maoni hayo yalipata kutolewa kwangu na Profesa E. Kezilahabi wakati alipousoma
mswada huu kwa mara ya kwanza.
2.
Hizi ni tenzi za Bahaya ambazo ni maarufu sana. M M.Mulokozi amefanya uchunguzi
mkubwa na mpana kuhusu tenzi hizo za Nanga katika tasnifu yake ya Udaktari
(Ph.D.) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
3.
Maelezo hayo yalitolewa kwangu na Daktari C. Ndulute ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi
katika Idara ya Fasihi ya Kiingereza ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
4.
F.E.M.K.Senkoro, Fasihi, Press and Publicity Centre, Dar es
Salaam 1984.
5.
E. Mphahlele, A Guide to Creative Writing, EALB, Dar es Salaam
1986.
6.
P. Muhando na N. Balisidya, Fasihi na Sanaa za Maonyesho, TPH,
Dar es Salaam: 1976.
7.
F.E.M.K.Senkoro, Riwaya ya Kiswahili na Maendeleo ya Umma, (Tasnifu
ya M A. ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1978)
8.
J. Berg Esenwein, "Writing the Short Story." A Practical
Handbook on the Rise, Structure, Writing and Sale of Modern Short Siory,Hinds,
Nobe and Eldredge - New York: 1909.
9.
R. Finnegan, Oral Literature in Afnca, Oxford
University Press: 1970
10.
Kama Na 8. 11 Kama Na. 6.
12.
Kama Na. 6.
13.
R. Scholes and Kellog, R., The Nature of Narrative, Oxford
University Press, New York: 1986.
14.
Kama Na. 4.
15.
P. Mbughuni, From Oral to Written- The Politicization of Kiswahili
Literature, Ph.D. Thesis, University of Indiana: 1978.
16.
R. Ohly, Aggressive Prose, TUKI, Dar es Salaam: 1981.
17.
Kama Na. 8.
18.
Kama Na. 8.
19.
E.A. Poe, On the Aim and Technique of the Short Story, Thomas
Y Crowell & Co., New York: 1902.
20.
J.H. Smith na Parks E.W., The Grat Critiques: An Anthology of Literary
Criticism, W.W. Norton & Co Inc. Vail Ballow-Press; 1978.
21.
W. Saroyan katika Steinberg, S.H. (Ed.) (et al.) Cassell's
Encyclopaedia of Literature (In two volumes: Volume 1), Cassell &;
Company Ltd, London: 1953.
22.
W. Blair (na wenzake), "Introduction to Short Stories, Drama and
Poetry," katika Literature, Scott, Foresman and Company,
1959: 1966 338